MKUU wa Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi, Filbarto Sanga, amewaonya baadhi ya watumishi wanaotumia nafasi zao kuomba fedha kwa wakandarasi au mafundi wanapotekeleza miradi, kwani vitendo hivyo vina athari kwenye utekelezaji wa miradi.
Sanga ametoa onyo hilo katika kikao cha kuandaa mpango mkakati wa ujenzi wa vyumba vya madarasa 23, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, kilichowakutanisha watendaji wa kata,watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji, walimu, wakuu wa shule na wakuu wa idara mbalimbali.
Amesema tabia hiyo husababisha baadhi ya miradi kusuasua, kutokana na fundi kubaki na kiasi ambacho hakikidhi kuwalipa mafundi wasaidizi, hivyo amewataka kuacha, kwa kuwa ni suala ambalo linaiaibisha halmashauri, huku akiziagiza idara zote zinazohusika na ujenzi huo kuhakikisha zinasimamia kikamilifu, ili madarasa yawe na ubora unaotakiwa.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha Sh milioni 460, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 23, ikiwa ni maandalizi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
Katika hatua nyingine DC Sanga ametoa wito kwa wananchi wilayani humo kuendelea kujitolea nguvu kazi, sehemu zinapojengwa shule hizo, kwani nia ya serikali ni kuwaondolea baadhi ya changamoto, ikiwemo ya kutembea umbali mrefu watoto wao.