Watumishi wasioenda likizo wanaiibia serikali
WATUMISHI wameonywa kuacha tabia ya kutokwenda likizo kwani kufanya hivyo ni kuiibia serikali.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Utumishi Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Fortunatus Mabula wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na Chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU).
Mabula alisema baadhi ya watumishi wamejijengea utaratibu wa kutokwenda likizo na uchelewaji kazini na kusema huo ni ukosefu wa nidhamu kiutumishi.
Pia álisema Talgwu kuwa Wilaya ya Kongwa imekuwa ikikosa ruzuku kutoka chama hicho hali inayofanya kushindwa kuendesha vikao vya robo mwaka.
Alisema serikali iliagiza mfanyakazi anapostaafu atalipwa pensheni ya asilimia 33 ambayo atalipwa kwa mkupuo halafu baada ya hapo atakuwa akipokea kiasi cha fedha kila mwezi kwenye asilimia 67 iliyobaki.
Godson Risasi akizungumza kwa niaba ya Kaimu Katibu wa Talgwu Mkoa wa Dodoma, álisema chama hicho kimefungua ofisi ya wanasheria wa kanda kwa ajili ya kushughulikia kesi za watumishi wanazopata wakiwa kazini.
Risasi alisema wanasheria hao watalipwa kutoka kwenye asilimia mbili ya mishahara wanayokatwa watumishi waliojiunga na chama hicho.
Pia Risasi aliwakumbusha watumishi kuwa wanapodai haki zao kutoka kwa waajiri wakumbuke kutimiza wajibu na majukumu yao kutokana na miongozo ya kazi waliyopewa.
Alisema kuwa Talgwu ipo kwa ajili ya kutetea na kulinda haki za wafanyakazi.