KAMANDA wa Polisi mkoani Geita, Safia Jongo amebainisha kuwa tathimini inaonesha dhana potofu ya kuua ndugu ili kupata mali (kafara) ni miongoni mwa kiini kinachochangia matukio ya kikatili mkoani hapa.
Kamanda Jongo amebainisha hayo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Lwamugasa, Kata ya Lwamugasa wilayani Geita na kueleza jeshi la polisi limejipanga kukomesha.
Amesema dhana potofu ya watu kuaminishwa kwamba wakiua ndugu zao watapata mali imesababisha watu kufanya ukatili kwa watoto na wazazi wao, hali inayoendelea kuchafua taswira ya Mkoa wa Geita.
“Yaani sijui nani kawaambia eti ukiua ndugu yako utapata mali, utapataje hiyo mali wakati utaishia jela, utaipataje mali kwa kuua baba yako, kwa kuua mama yako kwa kuua ndugu yako.
“Unaua huyo mtu kwa sababu mganga wa kienyeji kakuambia, huo ni ukatili kwa sababu mali utaipata kwa kufanya kazi kwa bidii siyo kwa kuua ndugu yako, siyo kwa kuua mama yako.
“Halafu mna tabia ya kuua mama yako kisa wachawi, angekuwa mchawi si angekuua zamani huko tangu ukiwa mdogo, leo umekuwa mtu mzima unasema mama mchawi, baba, mchawi.
“Unatengeneza mpango kazi unaua ndugu yako, mwisho wa siku Geita inaonekana haikaliki kumbe ni imani potofu, na imani mbaya na ukatili uliopitiliza ndio unafanya Geita yetu kuchafuka,” amesema.
Amewaonya waganga wa kienyeji wanaofanya ulaghai huo kuacha mara moja, kwani jeshi la polisi limejipanga kuwasaka na kuwachukulia hatua wote wanaofanya ramli hatarishi ndani ya jamii.
Pia amekemea wote wanaojichukulia sheria mkononi kwa kuwaua watuhumiwa wanaoachiwa kwa dhamana, kuacha kwa kuwa wanakiuka sheria kwani dhamana ni haki ya mtuhumiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amewataka wananchi kuheshimu malekezo ya viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, ili kuimarisha amani na kuruhusu miradi ya maendeleo kufanyika.