MKUU wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, Joshua Matagane, amewaonya wananchi wa Kata ya Shanwe, kuacha mara moja kuendelea kuuza na kujenga katika eneo la chuo hicho, wakati serikali imeshawalipa fidia.
Matagane ametoa onyo hilo akiwa eneo la soko la Shanwe, katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf, kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo na kuwaeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Ameiambia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kuwa, serikali tayari imeshawalipa fidia wananchi 33, lakini licha ya kulipwa bado wapo baadhi wanaendelea kuwauzia wananchi maeneo hayo, hali inayosababisha kuibuka kwa migogoro mipya.
Amemuomba Mkuu wa Wilaya kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa, ambao wamekuwa wakihusika kutengeneza migogoro hiyo kwa kushiriki kuuza maeneo hayo, hali ya kuwa wanafahamu ni mali ya chuo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf amewataka wataalamu na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mpanda, ndani ya siku saba waweke kambi katika kata hiyo na kuhakikisha wanapitia maeneo yote yenye migogoro pamoja na kutoa elimu, ndani ya muda huo ripoti imfikie ya nini kifanyike.
Amemuagiza pia Mkurugenzi kutekeleza agizo la kuhakikisha maeneo yote ya taasisi za serikali yanawekewa mipaka, ikiwa ni pamoja na kuwataka wananchi kutoendelea na shughuli zozote katika maeneo yenye migogoro, mpaka pale utatuzi utakapokuwa umetolewa.