WAVULANA 15 wanaodaiwa kujihusisha na makundi ya uhalifu kwa kupora mali za watu na kujeruhi mkoani Katavi wamekamatwa na polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ya mafanikio ya jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi Februari hadi Machi, ameyataja makundi hayo tishio kuwa yanajiita kwa majina ya Damu Chafu, Manyigu na Kaburi Wazi.
Amesema chanzo cha kuzuka makundi hayo ni malezi mabovu ya wazazi na kushindwa kuwafundisha maadili mema.
Amesema baadhi ya waliokamatwa ambao wengi ni watoto chini ya umri wa miaka 18 tayari wamefikishwa mahakamani.
Ameonya kuwa polisi itachukua hatua kwa wazazi ambao watoto wao watakamatwa kwa matukio ya uhalifu.
Aliyataja mafanikio mengine yaliyopatikana kwa kipindi hicho ni kukamata watuhumiwa 14 wa makosa mbalimbali ya kukutwa na mali za wizi.
Pia Polisi Mkoa wa Katavi, imewafikisha mahakamani watu wawili Omary Lukele (56) na Denis Devis (44), wote wakazi wa Kigoma wakiwa na vipande sita vya meno ya tembo, pia wamewakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 10 baada ya kukamatwa na silaha 7 aina ya gobori.