Wavuvi kupatiwa boti za kisasa

SERIKALI imetenga fedha kwenye Programu maalum ya mkopo wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kupitia dirisha la extended credit facilities (ECF) kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi boti za kisasa.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega Bungeni jijini Dodoma leo Mei 19, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge Aida khenan wa Nkasi kaskazini, aliyehoji mpango wa serikali katika kuwapatia wavuvi wa Ziwa Tanganyika zana za uvuvi za kisasa.

Ulega amesema katika kutekeleza mpango huo, Serikali inakamilisha taratibu za kutoa boti 158 kwa mkopo kupitia Benki ya Kilimo (TADB) kwa vyama vya ushirika 45, vikundi vya wavuvi 71 na watu binafsi 43.

Advertisement

Aidha, katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika jumla ya vyama vya ushirika vine, vikundi vinne na watu binafsi watano, wanatarajiwa kunufaika na mkopo wa boti hizo usio kuwa na riba.

Amesema Serikali kupitia (TADB) inatoa mitaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili kuboresha shughuli zao za maendeleo.

Aidha, Serikali inawahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi, SACCOS na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana na vyombo bora vya uvuvi.