Wavuvi waomba elimu ya uokozi majini
WAVUVI katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma wameomba kupewa elimu ya uokozi iwasaidie inapotokea dhoruba na vyombo vyao kuzama majini.
Katibu wa Chama cha Wavuvi Mkoa wa Kigoma, Mohamed Kasambwe alisema hayo wakati taasisi ya African Relief ilipokuwa ikikabidhi mitumbwi tisa kwa ajili ya kuvulia kwa wavuvi wa mwalo wa Kibirizi mjini Kigoma.
Kasambwe alisema inapotokea dhoruba ndani ya ziwa kwa boti au meli kupata majanga ya kuzama, wao ndiyo wanakuwa karibu kwa sababu muda mwingi wapo ndani ya ziwa hivyo misaada ya vifaa hivyo iende sambamba na elimu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mitumbwi hiyo, Msimamizi wa miradi ya taasisi hiyo kwa mkoa Kigoma, Gwanko Kamana alisema kukabidhiwa mitumbwi hiyo kunatimiza idadi ya mitumbwi 24 yenye thamani ya Sh milioni 60 ambazo taasisi hiyo imekabidhi kwa wavuvi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika mjini Kigoma.
Msimamizi huyo wa miradi ya African Relief Organization mkoa Kigoma, alisema mitumbwi imekabidhiwa bila kujali itikadi zozote.
Wamekabidhi mitumbwi tisa kwa wavuvi wa eneo la Kibirizi ikiwa ni kukamilisha mitumbwi 24 iliyotolewa na taasisi hiyo yenye thamani ya Sh milioni 60 ikilenga kuongeza shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa Kigoma.
Akizungumza katika makabidhiano hayo,Shehe wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa aliwataka wavuvi waliokabidhiwa mitumbwi hiyo kuifanyia kazi na kuleta matokeo kama ilivyokusudiwa ili kuwatia moyo wafadhili hao waweze kusaidia watu wengine zaidi.
Kiburwa alisema matumizi mabaya ya misaada inayotolewa na wahisani mbalimbali inakatisha tamaa na kufanya watu wengine kushindwa kufaidika.