Wawekaji matuta barabarani waonywa Shinyanga
MENEJA ya Wakala wa Barabara (Tanraods) mkoani Shinyanga Injinia Mibara Ndirimbi amewataka wananchi wa maeneo ya vijijini kuacha kujichukulia sheria kiholela juu ya uwekaji matuta kwenye barabara za changarawe.
Injinia Ndirimbi ameyasema hayo jana katika ziara na waandishi wa habari ya kutembelea miundombinu ya barabara huku akieleza uwekaji wa matuta una utaratibu wake kisheria na kuweka kiholela ni kukiuka.
“Ninawaomba wananchi wa kijiji cha Mwabomba muone namna ya kudhibiti madereva wanaoendesha mwendokasi muwatumie viongozi wa vijiji na kata muweze kupitisha sheria ndogondogo za kuwalinda ili kuthibiti madereva wanaokwenda mwendokasi sio kuweka matuta.”amesema.
Amesema Sh billioni 13.38 zilitengwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023 na Sh billioni 2.69 zilitoka kwenye mfuko wa barabara (Road Fund) kwaajili ya miradi ya maendeleo na tayari makaravati mapya yamejengwa kwenye maeneo korofi.
Injinia Ndirimbi amewashauri wananchi wanapotaka kujenga makazi ya kudumu wahakikishe wanaacha mita 30 kila upande kwa ajili ya hifadhi ya barabara na kuheshimu mipaka iliyowekwa.
Amesema changamoto iliyopo baada ya matengenezo ya barabara mifugo kukupitishwa na kuharibika kwa haraka kwani ikipitishwa zile kwato za ngo’mbe zinachimba barabara pia wengine wamekuwa wakilima kandokando ya barabara.
Ernet Mpema amesema kabla ya maboresho daraja linalounganisha Wilaya ya Mbogwe Mkoa wa Geita na kijiji cha Mwabomba Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama lilikuwa lina jaa maji na watu walikuwa wakitumia fursa ya daraja hilo kipindi cha masika kuwavusha watu na kuwapa hela.