Wawekezaji 27 wapatikana malazi hifadhini

DODOMA; SERIKALI imesema Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limeendelea na juhudi za kuvutia wawekezaji katika huduma za malazi, ambapo wawekezaji 27 wamepatikana na wanaendelea na ujenzi.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Mei 31, 2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

“Katika hatua nyingine, Shirika limeendelea na jitihada za kuvutia wawekezaji katika huduma za malazi ambapo wawekezaji 27 wamepatikana na wanaendelea na ujenzi.

“ Aidha, jumla ya huduma za malazi (loji 4, kambi za kudumu 23) zenye vitanda 1,148 zinajengwa katika Hifadhi za Taifa 5: Serengeti 780, Ruaha 170, Tarangire 100, Saadani 50 na Mikumi 48.

“Sambamba na hilo, Shirika linaendelea na ujenzi wa nyumba 3 za kulala wageni za gharama nafuu zenye jumla ya vitanda 178 katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Mikumi na Ruaha; hosteli katika Hifadhi za Taifa Ruaha, Mikumi, Saadani na Nyerere; pamoja na vituo 3 vya kutolea taarifa katika Hifadhi za Taifa Serengeti, Ruaha na Mikumi,” amesema Waziri Kairuki.

Habari Zifananazo

Back to top button