Wawekezaji kimkakati ruksa kuomba uraia

DODOMA: SERIKALI imesema ipo tayari kutoa uraia kwa wawekezaji wa miradi ya kimkakati.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa msimamo huo bungeni Dodoma jana kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa hapo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Janet Mahawanga (CCM). Mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini serikali itaboresha sheria za uhamiaji ili kuweka urahisi kwa wawekezaji wa kimkakati kupata uraia kutokana na heshima ya uwekezaji wao kwa taifa kama wafanyavyo mataifa mengine.

Majaliwa alisema serikali inawapa fursa wawekezaji hao ahueni ya kikodi, kibiashara na kuwapa ushirikiano katika uendeshaji na wanapoishi kwa miaka 10 wanapata nafasi ya kuomba uraia.

“Mradi tu anapopata uraia, lazima akubali kuendelea kuwa Mtanzania, lakini pia awe miongoni mwa watu wanaochangia uchumi na hayo yote yanapofikishwa uhamiaji hakuna shida kwa sababu wanasimamiwa na TIC (Kituo cha Uwekezaji Tanzania),” alisema.

Majaliwa alisema serikali ina mifumo na sheria za uhamiaji kama nchi nyingine na kwamba sheria zinaruhusu watu kutoka nje kwa vibali maalumu na shughuli mbalimbali.

Alisema uwekezaji wa kimkakati hauwezi kuwa wa mwaka mmoja, miwili, mitatu au minne hivyo wawekezaji wa miaka 10 ni wale ambao wameishi nchini kwa muda mrefu na wanahitaji uraia.

“Tunapojiridhisha huyu ni mwekezaji wa mradi mkubwa wa gharama kubwa na wa muda mrefu, wanahitaji usimamizi wa karibu, hao nao tumewafungulia dirisha lao la kuona umuhimu wa wao kuwa sehemu yetu,” alisema Majaliwa.

Aliongeza, “wapo ambao wanakuja kwa lengo la utalii, wapo ambao wanakuja kikazi, wapo ambao wanakuja kwa uwekezaji… serikali yetu imeweka sheria lakini imefungua milango ya wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali.” Majaliwa alisema serikali imewaweka wawekezaji hao kwenye madaraja wakiwamo wenye miradi ya kimkakati. Alisema miradi hiyo ni ya gharama kubwa na ya muda mrefu na kwamba serikali imeweka sheria ambazo mwananchi yeyote kutoka nje anazifuata kama anataka kuishi nchini. “Serikali tumeweka eneo ambalo mwananchi yeyote kutoka nje anataka kuishi nchini afuate sheria zetu, moja kati ya sheria zetu awe ameshaishi nchini kwa miaka 10,” alisema Majaliwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button