Wawekezaji wahakikishiwa mazingira mazuri
DSM; KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk Hashil Abdallah, amesema Ofisa yeyote wa Serikali atakayekwamisha ufanyaji biashara, uwekezaji au uanzishwaji viwanda nchini ni adui namba moja wa serikali na atachukuliwa hatua za kisheria.
Vilevile, ametoa wito kwa watendaji kuwezesha uwekezaji, ufanyaji biashara, uanzishaji viwanda na kuhakikisha kila mwekezaji anapata anachostahili kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Dk Abdallah ameyasema hayo wakati akiongoza Kamati Maalum ya Katibu Mkuu Kiongozi inayojumuisha Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Viwanda na Biashara, Fedha, Mipango na Uwekezaji, Kilimo na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera walipotembelea Kiwanda Cha sukari mkoani Kagera kuona hali ya uwekezaji na kutatua changamoto walizonazo.
Aidha, Dk Abdallah amesema Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameweka sera na mazingira wezeshi katika ufanyaji biashara uwekezaji na uanzishaji wa viwanda ili kuiwezesha Tanzania kujitosheleza katika mahitaji ya bidhaa muhimu na kuuza ziada nje ya nchi na kutimiza malengo ya Tanzania kuilisha Dunia.
Akifafanua zaidi, amesema serikali imeanza kutimiza malengo hayo kwa kuanza na eneo la sukari, ambapo Kiwanda cha Sukari cha Kagera kina uwezo wa kuzalisha tani 150,000 kwa mwaka katika mwaka 2023/2024 na kinapanga kuzalisha tani 300,000 kwa mwaka kitakapokamilisha upanuzi wa awamu ya nne na hivyo kuchangia kuifanya Tanzania kutoagiza sukari nje ya nchi, kuongeza ajira na pato la taifa hususani fedha za kigeni.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Tobi Nguvilo amesema uongozi wa mkoa huo uko tayali kumlinda, kumtunza, kumsaidia na kuhakikisha hakwami kwa jambo lolote mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera kwa kuwa mkoa huo unakitegemea kiwanda hicho kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii kwa kuajiri wananchi 115,000 kutoka mkoani humo pamoja na utoaji wa huduma bora za shule na hospitali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Sukari na Mmiliki wa Kiwanda cha Sukari Kagera .Seif Ally Seif amesema anaunga mkono juhudi za serikali katika kuwawezesha wawekezaji, ili kutimiza dhamira ya kuiwezesha Tanzania kuilisha Dunia kwa kuanza na sekta ya sukari inayotoa ajira nyingi na kuongeza pato la taifa zikiwemo fedha za kigeni.