Wawekezaji wazawa waahidiwa mazingira mazuri
KAMATI ya kudumu ya Ustawi wa Maendeleo ya Jamii pamoja na Taasisi ya OSHA wamefanya ziara kwenye kiwanda cha Azam kinachozalisha unga na kiwanda cha Lodhia cha kuzalisha nondo kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa sheria ya usalama na afya mahali pa kazi.
Ziara hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam Agosti 26, 2023 ikiwa na lengo la kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wa sekta binafsi kwa ajili ya kuwezesha biashara nchini.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Maendeleo ya Jamii, Fatuma Hassan amesema wawekezaji wa sekta binafsi wakipata fursa wataongezeka zaidi Afrika na nje ya Afrika na kushauri serikali kuweka mazingira bora zaidi kwa wawekezaji wazawa, ili kuongeza ajira nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Prof.
Jamal Katundu amesema watahakikisha wawekezaji wanawekewa mazingira mazuri ya kufanya kazi ikiwa na kuwahisha kupewa mapema.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako ametoa pongezi kwa mfanyabiashara Said Bakhresa kwa kutoa ajira kwa kiwanda hicho kwa watu 8,000 na wa wajasiriamali 20,000 kwa namna mbalimbali.
Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda anasema mkono wa OSHA umehusika kuhakikisha viwanda vya ndani vinakua, kwa vile wanawakagua, na kushauri namna ya kulinda wafanyakazi na kutoa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana nao.