Wawili jela maisha kilo 20 za heroin

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imewakuhumu kifungo cha maisha jela washitakiwa Silvani Makasanga maarufu Kelvin na Ali Juma  baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 20.24.

Mahakama hiyo pia iliagiza kuteketezwa dawa zilizokamatwa na pia gari lililokuwa linatumika kusafirisha dawa hizo lirudishwe kwa mmiliki wake.

Hukumu hiyo ilisomwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Jaji Mustapha Ismail, mahakama hiyo ilipoketi mkoani Morogoro.

“Nimesikiliza na kutafakari hoja za pande zote mbili na kwa mwongozo wa sheria kwamba sheria haiwezi kubadilika badilika, sheria inataka mtu aliyetiwa hatiani kwa makosa haya afungwe maisha. Kwa kesi hii nawafunga washtakiwa kifungo cha maisha jela kuanzia tarehe ya uamuzi huu,” alisema Jaji Ismail.

Alisema kwa mujibu wa maelezo ya awali waliyosomewa washitakiwa, ilidaiwa kuwa walitenda kosa hilo Aprili 29, 2021 walipokamatwa katika kituo cha ukaguzi cha Sangasanga, Mvomero mkoani Morogoro baada jeshi la polisi kutonywa kuwa kuna gari aina ya Toyota Noah yenye namba T 421 DEA likitokea Ruvuma kwenda Dar inahisiwa kubeba dawa za kulevya.

Jaji Ismail alisema kwenye maelezo hayo ilielezwa kuwa Jeshi la Polisi kwa kutumia intelijensia walijipanga na kufanikiwa kulikamata gari hilo na kulikagua, walikamata  kiroba kilichokuwa na paketi 20 za unga ndani yake ambao ulidhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.

Baada ya ukaguzi na mahojiano mshtakiwa wa kwanza (Kelvin)  alikiri kumiliki mzigo huo na kusema kuwa paketi tano alikuwa akizipeleka Chalinze kwa mshitakiwa wa pili (Juma).

Alisema mpango ulisukwa, Kelvin akaendelea kuwasiliana na Juma mpaka alipokamatwa  Chalinze, baada ya kukamatwa walienda naye nyumbani kwake Tanga kufanya ukaguzi lakini hakukutwa na kitu ingawa wakati wa kuchukuliwa maelezo ya onyo Juma alikiri kuhusika.

Wakati  wa kusikiliza ushahidi upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa serikali Mosses Mafuru na Nestory Mwenda ambao walipeleka mashahidi 9 na vielelezo 8, upande wa utetezi uliwakilishwa na mawakili Mkilya Daudi na Salim Gogo ambao hawakuwasilisha kielelezo chochote.

Katika hukumu hiyo Jaji Ismail alisema washtakiwa wenyewe katika maelezo yao ya onyo walikiri na kwamba mshtakiwa wa kwanza ndiye aliyesaidia kukamatwa mshtakiwa wa pili ambaye naye alikiri kuhusika.

“Hii inaonesha kwamba Kelvin alikuwa na mawasiliano na Juma, swali linabaki ni je ushahidi uliotolewa unaweza kuwatia hatiani?,” alisema.

Alisema kutokana na ushahidi ulitolewa, ulikuwa ni ushahidi wa moja kwa moja na si wa kusikia hivyo mahakama ilijiridhisha kuwa hakuna mwanya wowote unaoweza kutikisa ushahidi wa mashtaka ambao umejengwa katika msingi imara hivyo mahakama iliwatia hatiani.

Habari Zifananazo

Back to top button