Wawili mbaroni utengenezaji noti bandia

SONGWE: JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kosa la kutengeneza na kukukutwa na noti bandia za nchini Zambia.

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, ACP Theopista Mallya wakati akiongea na vyombo vya habari, leo Oktoba 03, 2023 katika Ofisi za Jeshi la Polisi.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 19,2023 Mtaa wa Nazareth, Kata ya Mwakakati mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba wakiwa na noti 12 za nchini Zambia zenye thamani ya Kwacha 50.

“Ni kwamba walikamatwa wanaume wawili, mmoja ni Mkulima mkazi wa Mpulungu Zambia mwenye umri wa miaka 48 raia wa Zambia na mwenzake Mkulima mkazi wa Msongwa Tunduma mwenye umri wa miaka 59 raia wa Tanzania,” alisema Mallya.

Kamanda Mallya alisema pia walikamata karatasi 10 zenye ukubwa wa A4 zikiwa zimechapishwa Kwacha 50 kwa idadi ya noti 36 ikiwa ni pamoja na karatasi ya A4 moja iliyochapishwa noti nne zenye thamani ya kwacha 100.

Aidha watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na visu viwili vikubwa, kisu kingine kidogo cha kukunja, mkasi mmoja wa kukatia karatasi pamoja na vitambulisho viwili vya Taifa la Zambia vyenye namba Z.17714847 na Z.1600353.

Mkurugenzi wa Benki Kuu (BOT) tawi la Mbeya, James Machemba alisema tukio hilo la utengenezaji fedha bandia ambazo hutumika katika mpaka huo kuwa ni uhujumu uchumi ambapo huathiri uchumi wa Mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Alisema wamekuwa wakishirikiana na wenzao wa Zambia kutoa elimu kwa Wananchi na wafanyabiashara wanaofanya biashara za kubadilishana fedha ili waweze kuzitambua fedha bandia.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button