Wawili wafa kwa radi wakiangalia Afcon Morogoro
WATU wawili wamekufa kwa kupigwa na radi wakati wakiangalia mashindano ya 34 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) hatua ya robo fainali katika kitongoji cha Kungwe kijiji cha Kigugu Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro usiku wa jana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alisema hayo Februari 3, 2024 kuwa tukio hilo lilikotea Feruari 2, mwaka huu majira ya usiku.
Mkama alisema watu hao wawili walikuwa sabuleni usiku wakiangalia televisheni mashindano ya mpira wa miguu ya Afcon wakati mvua ilikuwa ikinyesha ambayo iliambatana na radi .
Aliwataja waliofariki dunia walitambuliwa kuwa ni Juliana Robert Albat (31), mkazi wa Kungwe na mwingine ni Mateso Athanas Elnordin (35) pia mkazi wa Kungwe , wilayani Mvomero.
Kufuatia tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa aliwashauri wananchi kuchukua tahadhari nyakati za mvua zinaponyesha zinazoambatana na radi kwa kuzima umeme na vifaa vingine vya mawasilino ikiwemo simu na TV ambavyo vinaweza kuingiliana mawimbi ya radi ili kuepuk madhara yanayoweza kujitokeza nyakati hizo .
Februari 2, 2024 ilianza michuano ya hatua ya robo fainali ya mashindano hayo majira ya saa mbili usiku kati ya timu ya Nigeria au Super Eagles dhidi ya timu ya Angola ambapo Nigeria waliibuka na ushindi wa bao 1-0 , na mchezo uliofuatia majira ya saa tano usiku ulikuwa kati ya Jamhauri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) dhidi ya Guinea ambapo DRC waliibuka kidedea kwa mabao 3-1