Wawili wahukumiwa kunyongwa

WATU wawili wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa kukusudia Gervas Mgonja kwa kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Washitakiwa hao ni Amidu Mbegu (40) na Amiry Chiwaka (28), wote ni wakazi wa Dar es Salaam.

Washitakiwa hao walisomewa hukumu hiyo na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu.

Akisoma maelezo ya ushahidi, Ruboroga alisema kuwa wakiwa katika maeneo ya Zingiziwa Chanika, washitakiwa hao walimshambulia Mgonja kwa mapanga na kumuua na kisha kutupa mwili wake kwenye shimo lenye futi sita lililokuwa limechimbwa kwa ajili ya kufyatulia matofali, umbali wa mita 15 kutoka eneo walipofanya shambulio hilo.

Kwa mujibu wa ushahidi, Januari 12, mwaka 2016, Mbegu alikutana na Chiwaka saa 10:00 jioni nyumbani kwa rafiki yao aliyefahamika kwa jina moja la Kijagi.

Akawaeleza kwamba ana ugomvi na mpenzi wake Ilima Simon kwa sababu ana mahusiano ya kimapenzi na mwanaume aitwaye Fundi na kukubaliana kumsaka.

Walikubaliana kumpiga mapanga Fundi na ilipofika saa 1:00 usiku, siku hiyohiyo, Mbegu alitangulia nyumbani kwa Ilima na kumkuta akiwa anakunywa pombe za kienyeji na Fundi pamoja na mteja, Gervas Mgonja, akawasalimia na kukaa mlangoni.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Ilima alipomwona Mbegu alimuuliza “umekuja kuniletea vurugu?” Mbegu akamjibu kwamba pale ni klabuni amefuata pombe.

Alidai kuwa baada ya muda mfupi alikuja Chiwaka akiwa na mapanga mawili, Fundi alipoyaona mapanga alikimbia huku akifukuzwa na marafiki zake Mbegu ambao ni Bojo na Kijagia. Hata hivyo, hawakufanikiwa kumkamata.

Kwa upande wa Mbegu alimkimbiza Gervas Mgonja na kufanikiwa kumkata na kuamuru akae chini na ndipo Mbegu na Chiwaka waliungana na kumshambulia kwa mapanga na kusababisha kifo chake.

Habari Zifananazo

Back to top button