Wawili wapoteza maisha wakidhaniwa kula chakula chenye sumu

MWANZA: KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema kuwa watu wawili wa familia mbili tofauti wamepoteza maisha wakidhaniwa kula chakula chenye sumu.

 

 

Advertisement

Kamanda Mutafungwa amesema, tukio hilo lilitokea Desemba 17, 2023 ambapo Maua Mwilikwa (10) mkazi wa Mabatini amepoteza maisha katika hospitali ya Bugando jijini Mwanza, majira ya saa 11:00 alfajiri na Thomas Thomas (18) mkazi wa Mabatini amefariki katika hospitali ya Sekou Toure ya jijini Mwanza, majira ya saa 10:00 jioni akipatiwa matibabu.

 

 

“Watu hawa walifikishwa katika hospitali hizo kwa matibabu baada ya kuanza kutapika na kuharisha baada ya kula mboga aina ya uyoga aidha waliopoteza maisha wametoka katika familia mbili tofauti familia ya kwanza ya mzee Zuberi Msabaha (70) mkazi wa Mabatini Kaskazini ambapo amefariki mjuu wake aitwaye Maua Mwilikwa,” amesema

 

Aidha, Kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa familia ya pili ni ya Eva Jonas (47) mkazi wa Mabatini Mashariki, ambapo watu saba walikula mboga hiyo na baada ya muda mfupi walianza kutapika na kukimbizwa kituo cha afya cha Polisi Mabatini ambapo baada ya hali zao kutoridhisha walipelekwa Hospitali ya Sekou Toure kwa matibabu zaidi ambapo Thomas Thomas ambaye ni mtoto wa Eva Jonas alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu.

 

 

Waathiriwa wengine wanaoendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Bugando ni Maua Ibrahimu (56) mkulima na mkazi wa Mabatini, Eva Jonas (47) mkazi wa Mabatini, Edina Thomas (20), John Thomas (15), Tomision Thomas (13) mwanafunzi wa kidato cha kwanza Mtoni Sekondari Grelious Simon mwaka (1) na Alfani Selemani (14) mwanafunzi huku hali zao zikiendelea vizuri.

 

Pia Kamanda Mutafungwa amesema kuwa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linaendelea na jitihada za kumtafuta mtu aliyeuza uyoga huo ili aweze kuhojiwa pia kamanda Mutafungwa ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa huo kuwa makini na baadhi ya vyakula visivyofaa.

4 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *