Wazabuni umeme vijijini wabanwa

WAKANDARASI waliopewa zabuni za kusambaza umeme vijijini na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), wamekalia kuti kavu baada ya serikali kusema hairidhishwi na kasi na mwenendo wa utekelezaji kazi hiyo.

Aidha serikali imetoa siku saba kuanzia sasa kwa wakandarasi wanaosuasua kuwasilisha mpango kazi wao wa kujikwamua REA na kuwa baada ya mwezi serikali itawapitia kuangalia utendaji wao.

Pia imesema baada ya miezi miwili kuanzia sasa itaanza kutumia utaratibu mpya wa kutoa zabuni kwa wakandarasi na yule ambaye atakuwa hajatekeleza kazi ya zabuni aliyonayo kwa chini ya asilimia 60, hatapewa zabuni nyingine, lakini pia wale watakaokuwa wametekeleza vizuri watapewa kipaumbele kwenye zabuni nyingine.

Hayo yamebainishwa leo Dar es Salaa na Waziri wa Nishati January Makamba, wakati akizungumza na wakandarasi hao na kuwaeleza wazi kuwa serikali hairidhishwi na kasi ya kazi zao na kuwataka wajitathmini, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Niwaambie serikali haturidhishwi na kasi ya utekelezaji wenu wa miradi mliyopewa, baadhi yenu mmetelekeza site(maeneo ya miradi) na fedha mlizopewa kwa kazi hiyo mmepeleka kwenye mambo yenu mengine,” amesema na kuongeza:

“Nguzo za umeme mmezitelekeza kwenye vijiji hadi zimepasuka, mkizidi tutawafungulia kesi na mtafungwa , hatuna cha msalia mtume wala mzaha, na wale mnaosumbua tutawaengua tutawapeleka Bodi ya Usajili  Wakandarasi (CRB),wawaengue na hili nitasimamia mwenyewe, serikali haiwezi kulaumiwa na wananchi kwa uzembe wenu,fedha tumewapa kazi hazifanywi,”amesisitiza January.

 

Habari Zifananazo

Back to top button