Wazalishaji chumvi isiyo madini joto kuchukulia hatua
MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amewaagiza wakurungezi watendaji wa halmashauri kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wazalishaji wa chumvi isiyo na madini joto ya kutosha mkoani hapa.
Sambamba na hilo amewataka wakurungezi hao kusimamia na kuhakikisha kuwa chumvi zinazozalishwa na kusambazwa ndani ya mkoa zinafanyiwa uchunguzi wa kimaabara ili kubaini uwepo wa madini joto kulingana na miongozo ya serikali.
Abbas ametoa maagizo hayo leo Agosti 10 wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023.
Amesema kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi uliofanywa mkoani humu unaonyesha utumiaji wa madini joto ni asilimia 60 kwa kaya. Malengo yaliyowekwa na serikali ni kufikia asilimia 90 ya kaya.
Tafiti zinaonyesha kuwa jamii isiyotumia chumvi yenye madini joto ya kutosha ipo hatarini kupata madhara ya kuvimba kwa tezi la shingo, kuharibu mimba, watoto kuzaliwa na uzito pungufu.