WAZAZI nchini wameaswa wasiwadekeze watoto, ikiwa ni pamoja na kuzuia wasifanye kazi shuleni kwani ni hatari kwao siku za usoni.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Shule ya Msingi Rockeni Hill na Shule ya Sekondari Anderlek Ridges, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, Alexander Kazimili na kuongeza kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakisingizia watoto wao wana matatizo ya kiafya, ili tu wasifanye kazi shuleni.
Akizungumza leo katika mahafali ya 18 kwa shule ya msingi Rocken Hill na Shule ya Sekondari Anderlek, amesema hata wanapokuwa likizo nyumbani, baadhi ya watoto wamekuwa wakidekezwa na kutofanya shughuli yoyote, jambo ambalo ni hatari kwa mtoto.
“Wazazi tusitoe sana makucha kwa watoto hata pale hapastahili, muache ajifunze siku hizi vipaji vina fursa, sababu ajira ni chache na usimruhusu sasa alale huko huko na kujawa kiburi.
“Muongoze kwenye maadili usiwaachie walimu peke yao, shirikianeni mumuokoe mtoto,”amesema Kazimili.
Amesema wazazi wanapowadekeza watoto kupita kiasi, ndipo watawaingiza kwenye vitendo vya kuingia kwenye uhalifu na kuongeza kuwa wahakikishe wanawalea watoto katika maadili mema, wakifanyishwa kazi shule ni sehemu ya kujifunza.