JUMUIYA ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Arusha, imeanza maandalizi ya maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa CCM kwa kupanda miti kwenye kata tatu za Jiji la Arusha sanjari na utoaji wa semina kwa viongozi mbalimbali wa jumuiya hiyo.
Akiongoza wakati wa tukio hilo, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Wilaya ya Arusha, Ali Juma Mwinyimvua ‘Ally Meku’, amesema jumuiya hiyo inamuunga mkono Rais Samia katika kazi mbalimbali, ikiwemo kusemea masuala ya elimu, malezi na miradi inayotekelezwa na CCM.
Amesema miti hiyo iliyopandwa Kata ya Sinoni katika Shule ya Msingi Ukombozi, itakuwa mfano kwani shule hiyo imeonesha njia katika utunzaji wa mazingira sanjari na elimu bora.
“Wazazi tuzisemee kazi za Rais, sote tunaziona na nasisitiza tusimamie malezi kwa watoto wetu, lakini pia tumechukua changamoto ya ukosefu wa jengo la utawala shuleni hapa kama wazazi tunalifanyia kazi jambo hili,” amesema.
Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ukombozi, Fanuel Kighera, ameshukuru tukio hilo la upandwaji miti mbalimbali shuleni hapo na kukiomba chama kuwasaidia kupata jengo la utawala, kwani hivi sasa wanatumia darasa moja na kuligeuza ofisi kwa ajili ya walimu 61 kulitumia.
Pia wazazi hao wengine walijipanga Kata ya Levolosi na Kata ya Kati kwaajili ya kupanda miti.