Iringa wataka vita dhidi ya ushoga iongezwe

Iringa wataka vita dhidi ya ushoga iongezwe

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Iringa imewataka wazazi kushiriki katika vita dhidi ya vitendo vya ulawiti na ushoga vinavyoanza kuonekana kama vya kawaida katika baadhi ya jamii za kitanzania.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, ubakaji, ulawiti na kufanya mapenzi ‘kinyume na maumbile’ ni baadhi ya makosa ya jinai ambayo mtu akikutwa na hatia adhabu yake ni pamoja na kifungo jela.

Akitoa nasaha zake katika kikao cha Baraza Kuu la Jumuiya ya mkoa huo kilichofanyika leo mjini Iringa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kupitia jumuiya hiyo George Gandye alisema; “Vitendo hivi ni moja ya changamoto zinazotakiwa kushughulikiwa na jumuiya yetu.”

Advertisement

Aliwataka wanaume wa Iringa kukumbuka historia ya ujasiri wao na kuwa wa kwanza kuonesha kwa vitendo kutokubaliana na vitendo hivyo.

Awali Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Aggrey Tonga alisema jumuiya ya wazazi ina kazi kubwa ya kusaidia kuirudisha jamii ya Watanzania kwenye maadili, ambayo kuporomoka kwake kumechochea kuibuka kwa vitendo hivyo vya ulawiti na ushoga.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo alisema jumuiya yake imepanga kusaidia kutoa elimu ya afya ya uzazi, ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho kutokana na kuongezeka kwa vitendo hivyo.

Mbali na vitendo hivyo kukatazwa kwa mujibu wa sheria na maandiko matakatifu ya dini mbalimbali, alisema vina fedheha kwa jamii na moja ya sababu ya kukatisha ndoto za kimaisha za baadhi ya watu hususani watoto.

Ngajilo alisema wana kazi kubwa ya kufanya ili kuilinda jamii wakiwemo watoto hao dhidi ya ukatili wa kijinsia na mmomonyoko wa maadili na akaitaka jumuiya hiyo kubeba dhamana hiyo, kwani ni moja ya wajibu wake.

Katika kikao hicho ambacho pia kilitumika kutoa semina ya uongozi kwa viongozi wa jumuiya hiyo wa kutoka wilaya zote za Mkoa wa Iringa, Ngajilo alizungumzia ruhusa ya mikutano ya hadhara akisema ni wajibu kwa kila mwana CCM kufungua masikio yake na kusaidia kutoa ufafanuzi wa yale yatakayokuwa yanazungumzwa na wapinzani wao.

“Kazi ya kujibu hoja za wapinzani isiachwe kwa viongozi tu. Wanachama nanyi mna nafasi yenu, angalieni nini kimefanywa na kinaendelea kufanywa katika maeneo yetu, saidieni kuwaeleza wananchi,” alisema.