Wazazi waaswa namna bora ya kuwafunda watoto

DSM: KATIKA kuhakikisha watoto wanapata huduma za malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali kadiri ya taratibu za serikali, shirika la Children in Crossfire (CiC) linawajengea uwezo wamiliki na walezi wa vituo vya kulelea watoto wadogo na watoto wachanga (Day Care).

Akizungumza katika ufunguzi wa amafunzo hayo, Mratibu wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT -MMMAM) kutoka CIC, Frank Samsoni amesema fursa nzuri ya kujenga ubongo wa mtoto ni kuanzia miaka sifuri hadi miaka nane.

“Sensa ya mwaka 2022 inaonyesha watoto wapo milioni 16 idadi hiyo ni kubwa tofauti na nchi nyingine hii ni fursa tuwekeze kwa maisha ya badae.”Amesema Frank na kuongeza

“Mtoto ambaye anapata msingi mzuri mwanzoni ubongo wake unakuwa vizuri, lakini ukikosea tu ubongo wake unadumaa, hapo ujue hatengenezeki au utengeneze kwa gharama kubwa.”Amesema

Aidha amesema Dakika moja unayokutana na mtoto mdogo na kuzungumza nae, kuna mawili ama kumjenga ubongo wake au kumuharibu.

Kwa upande wa Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Baraka Makona serikali kwa kutambua vituo vya Day Care, tayari imezindua programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa lengo la kumaliza changamoto ya lishe duni na changamoto nyingine dhidi ya watoto hususani walio chini ya umri wa miaka nane.

Amesema, pamoja na mambo mengine, lishe duni inachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha lengo namba 3 kwa kuwakosesha watoto afya bora, na lengo namba 4 kwa kuwa kikwazo katika ujifunzaji wao.

“Vituo vilikuwa vinaendeshwa kiholela kila mtu na mfumo wake, tumetoa mwongozo ambao unafuatwa nchi nzima, kuanzia umri wa miaka sifuri miezi sita ya kwanza alelewe vipi kila umri muongozo umeeleza mpaka ufundishaji na nyimbo zao.”Amesema

“Nyie ndio mnakaa na watoto kwa muda mrefu kuliko wazazi wao ndio maana tunataka muwe na utambuzi wa kuwafahamu watoto vipaji vyao na changamoto zao, mfano kuna mtoto tulimbaini alikuwa anaelekea kwenye upofu lakini wazazi wake hawakujua hilo, sasa tunapaswa kuwa na walimu ambao wana utambuzi ili kuokoa changamoto za watoto.

“Kuna watoto wanakumbana na ukatili wa kijnsia, kuna watoto wanapata ulemavu lakini hiyo yote inatokana na kutotambulika haraka ili kupata usaidizi.”Amesema Makona.

Amesema, Mkoa wa Dar es Salaam unachangia pato la Taifa kwa asilimia 70 ya mapato yake hiyo inaonyesha kuwa watu wengi wapo ‘busy’ na shughuli zao na hivyo kuhitaji vituo vya Day Care kwa ajili ya watoto wao na kuwataka wamiliki na walezi kuzingatia weledi katika makuzi ya watoto na kwamba wapo kwenye mchakato wa kufuatilia kama mwongozo unatekelezwa.

Habari Zifananazo

Back to top button