Wazazi waonywa lugha chafu kwa watoto

WAZAZI na walezi wilayani Geita mkoani hapa wametakiwa kuacha tabia ya kutumia lugha na kauli chafu pale wanapowakemea watoto wao kwani zinatajwa kushadadia watoto kukosa maadili.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kalangalala mjini Geita, Costantine Lucas amesema hayo juzi wakati akitoa elimu ya kupinga ukatili kwa wakazi wa kata ya Ihanamilo mjini Geita.

Elimu hiyo ni sehemu ya Mradi wa Kumwezesha Binti Barehe Kubakia Shule (KAGIS) unaotekelezwa na shirika la RAFIKI SDO kwa ushirikiano na Plan International chini ya ufadhili wa watu wa Canada.

Advertisement

Costantine amesema kwa siku za hivi karibuni wazazi wengi wamebainika kutumia lugha ya matusi na vitisho wanapokemea watoto wao hali inayochangia ukatili wa kihisia na matatizo ya kisaikolojia.

“Kimsingi wazazi ambao wanatumia kauli mbaya ikiwemo kumuita mtoto wake mbwa, maana yake unamtengenezea baadaye awe anafikiria kama mbwa na unamtengenezea tabia za mbwa.

“Kwa hiyo wazazi waache kutumia hizi lugha, amkemee tu mtoto kwa lugha nzuri kama sehemu ya kuwahamasisha watoto ili baadaye nao wajisikie kabisa kwamba na wao wana wazazi

“Tunapotumia hizi lugha za matusi na lugha ngumungumu kihisia au kisaikolojia zina madhara makubwa, unaweza ukaona kama ni kitu kidogo sana kwa hiyo wazazi waache kutumia matusi na vitisho.”

Amesema kupitia mashindano ya mpira wa miguu yanayoratibiwa na mradi wa KAGIS elimu inaendelea kutolewa, mwamko wa kupinga ukatili umeonekana na wanaendelea kufichua aina zote za ukatili.

“Kupitia michezo hii mafanikio ambayo tunayapata kama serikali kwanza tumeweza kuwafikia watu wengi kwa maana watu wanaitikia kwa wingi na hivyo elimu imekuwa ni rahisi kwetu kuifikisha.”

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ihanamilo, Asterius Abbas amekiri mradi wa KAGIS umeleta mageuzi kwa watoto wa kike kusoma ambapo kwa mwaka huu asilimia 98 waliofaulu wanaendelea kusoma.

Mratibu Msaidizi wa Mashindano ya KAGIS kutoka RAFIKI SDO, Azory Baroha amesema mashindano yalianzia ngazi ya mitaa na kata na sasa yapo ngazi ya wilaya yakiambatana na elimu ya kupinga ukatili.

3 comments

Comments are closed.