Wazazi wapingwa watoto wadogo shule za bweni

WADAU wa elimu wamepinga utaratibu wa wazazi kuwapeleka watoto chini ya darasa la tano kukaa shule za bweni.

Hivi karibuni aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Francis Michael alisema Mwongozo wa Usajili wa Shule wa Mwaka 2020 unaeleza umri wa watoto wa shule ya msingi kulala bwenini kwa kusema hairuhusiwi kumlaza mtoto chini ya darasa la tano.

“Shule nyingi watoto wa darasa la pili na la tatu wamekuwa wakilazwa bweni huku wenye shule wakisema vikao vya wazazi vimeamua wakae bweni. Kuna umri ambao mtoto anapaswa kuendelea kukaa na mzazi apate malezi,” alisema Dk Michael.

Mhadhiri Msaidizi anayefundisha upimaji na tathmini katika elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mudhihir Mudhihir alisema kwa kuzingatia hali ya sasa na mmomonyoko wa kimaadili unahitajika usimamizi wa karibu kwa wazazi na walezi kuwalinda watoto.

“Saikolojia na kitaalamu, watoto wanapenda kujaribu jaribu vitu, kuelezeana tabia ikakua, hivyo wanaweza kuharibiana ukiwaweka wengi pamoja kusipokuwa na uangalizi wa karibu na uwezekano wa kueneza tabia mbaya unaweza kukua,” alisema Mudhihir.

Alisema tabia yoyote mtoto akiwa nayo kuanzia miaka sifuri hadi sita ni rahisi kuiendeleza hivyo unahitaji uangalizi wa wazazi baada ya kuwaachia jukumu hilo walimu au mtu mwingine.

Mwalimu Richard Mabala alishauri kama inawezekana serikali ipige marufuku watoto wa shule za msingi kukaa katika shule za bweni kwa kuwa wanahitaji uangalizi wa wazazi.

Mabala alisema watoto wanapopelekwa shule za bweni wanakosa fursa ya kujifunza mambo ya msingi kwa wazazi wao na wanakosa utulivu wa kisaikolojia kwa kuwa wanaamshwa mapema alfajiri na wanasoma hadi jioni.

“Ninachokiona mimi ni mashindano ya kimitihani sio sababu ya elimu. Hizi shule zinataka kuonekana zinafaulisha zaidi. Lakini kama shule mtoto atafundishwa vizuri mtoto atafaulu tu,” alisema.

Alihimiza wazazi wasikwepe jukumu la msingi la kuishi na watoto wao ili kuwafundisha mambo ya msingi ya maadili na kuwalinda dhidi ya vitendo viovu vikiwamo vya ulawiti na ubakaji.

“Kuna upweke mkubwa sana watoto kukaa bweni na wanakosa aina ya malezi,” alisema Mabala.

Mhadhiri mstaafu, Profesa Herme Mosha alisema maadili ya vijana huchangiwa na vyanzo vingi ikiwamo jamii alimozaliwa na kuishi kwa miaka mitano ya awali.

Meneja Mawasiliano wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Uwezo Tanzania, Grayson Mgoi alisema si sawa kwa watoto chini ya darasa la tano kuwekwa shule za bweni.

Mgoi alisema watoto wa umri huo wanahitaji kukaa mazingira ya nyumbani ili wacheze na wenzao na kukaa na wazazi badala ya kuanza masomo saa 12 asubuhi badala ya saa mbili asubuhi

“Huko shule za bweni hatamwona baba, mama, dada wala kaka mpaka pale atakaporudi likizo. Mtoto mbali na kujifunza darasani anapaswa kujifunza stadi nyingine mbalimbali,” alisema.

Mgoi alisema mtoto anahitaji kupata upendo wa baba na mama hivyo anapopelekwa shuleni mwalimu hawezi kuwa muda wote na watoto kwani anahitaji kufundisha zaidi.

“Huu utaratibu umeendana na biashara. Hata hii kulazimisha watoto wadogo wakae bweni ni biashara. Hii ni biashara tu za wenye shule wana majengo yao wanataka kupata faida. Hali hii ni kumchosha mtoto na kumuumiza,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button