Wazazi wasiohudumia watoto lawamani

MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amesema kuwa wazazi wanaoshindwa kuwahudumia watoto wao ndiyo wanaozalisha jamii isiyo na maadili.

Amesema kitendo cha wazazi kushindwa kuwajibika katika matunzo na malezi ya watoto wao imekuwa na mchango mkubwa kwa watoto hao kujitafutia mahitaji yao na kusababisha kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjifu wa maadili na uhalifu.

Alisema hayo wakati wa maadhimisho ya kimkoa ya siku ya Kimataifa ya Familia iliyofanyika manispaa ya Kigoma Ujiji na kusema kuwa madai ya   hali duni ya familia imekuwa ikichukuliwa na wazazi wengi kama sababu ya  kuacha kutekeleza matunzo na malezi ya watoto wao.

Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za Manispaa ya Kigoma Ujiji ambao walihudhuria maadhimisho ya siku ya Familia. (Picha zote na Fadhil Abdallah).

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kalli alisema kuwa jamii inao wajibu mkubwa wa kutafakari hatua za kuchukua katika kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo mmomonyoko wa maadili kwenye jamii na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.

Alisema kuwa pamoja na mikakati mbalimbali ambayo inatekelezwa mkoani humio kupitia Mpango wa Taifa wa kupinga Ukatili (MTAKUWA), bado vitendo vya ukatili vinaendelea mkoani humo, ambapo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita matukio 3260 yaliripotiwa.

Akitoa neno la tafakari katika maadhimisho hayo Katibu wa CCM Mkoa Kigoma, Mobutu Malima alisema kuwa wazazi wanapaswa kujitafakari kwa hali zote zinazotokea kwenye jamii kwa tabia, mila, mienendo na matendo yapo kwenye nafasi ipi katika kuwalea watoto.

Malima alisema kuwa matendo mabaya yanayofanywa na watu wengi chimbuko lake ni malezi ambayo watu hao walipata kutoka kwa wazazi wao, huku wengi wakiachwa kutolelewa kwenye misingi ya kumjua Mungu

Habari Zifananazo

Back to top button