WAZAZI nchini wametakiwa kuongeza umakini katika malezi ya watoto wao, ili kuwazuia kujiingiza kwenye magenge ya uhalifu.
Pia wameshauriwa kuwahamasisha watoto na masuala ya imani za dini, kwani ni msingi mzuri kwao kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu.
Ushauri huo umetolewa Dar es Salaam jana na Msemaji wa timu ya mpira wa miguu ya Ruvu Shooting iliyopo Ligi Kuu Tanzania Bara, katika mahafali ya darasa la saba Shule ya Msingi Blessed Hill, iliyopo Kitunda, Dar es Salaam.

Bwire aliyekuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi, wazazi, walimu na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo, aliwataka wazazi wa wanafunzi 202 wa darasa la saba wanaohitimu shule hiyo kuhakikisha wanaendeleza tabia nzuri waliyotoka nayo wanafunzi hao shuleni hapo.
“Shule ya Blessed Hill inasifika kwa kuwajenga vyema watoto katika maadili, naomba wazazi hawa vijana kuanzia Oktoba 6 mwaka huu watakapomaliza mitihani yao ya darasa la saba wanarudi mikononi mwenu, wasibadilike.
“Tuhakikishe tabia njema wanaendelea nayo, lakini tukiyumba tu katika malezi, basi ndiyo huko mtaani tunaunda magenge ya wahalifu, naomba na wazazi wengine wote wapokee salamu zangu. Tushirikiane kujenga jamii inayojitambua,” alisema Bwire na kushangiliwa.