LONGIDO, Arusha: WAZEE wa kimila wa Jamii ya Kimasai maarufu kwa jina la Laigwanani, Kata ya Engikaret, wilayani Longido, mkoani Arusha wametoa msaada wa vyakula, nguo, maji na vyombo vya kupigia kwa familia ya watu 11 waliokumbwa na mkasa wa nyumba zao kuchomwa moto.
Familia hizo zimekumbwa na dhahama hiyo mara mbili, Desemba 29 mwaka jana na tukio la pili limetokea Januari 26 mwaka huu.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amekiri kusikia tukio hilo na hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwasaka wale wote waliofanya tukio hilo.
Mongella amesema timu ya watalaamu imeshakwenda eneo la tukio na wanasubiri kujua tathmini ya nyumba zilizochomwa. Bado serikali inaendelea na uchunguzi, kuwabaini wahusika wa tukio hilo.
‘’Ni kweli tukio hilo liliwahi kutokea na sio kama serikali imekaa kimya iko kazini inafanyia kazi na wote waliohusika watachukuliwa hatua.’’ Amesema Mongella.
Awali akizungumza kwa niaba ya wazee wa mila, Laigwanani Elia Lukumay amesema wao wameamua kutoa msaada kwa familia hizo kwa kuwa serikali imekaa kimya bila ya kuwasaidia waliochomewa nyumba kwani hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao.
Lukumay amesema maboma matatu yamechomwa moto ikiwemo nyumba 11, mifugo ikiwemo mbuzi wadogo sita na kuku 18. Matukio yote mawili yamefanyika mchana majira ya saa 7 na saa 9 alasiri.
Vitu vilivyotolewa na wazee hao ni pamoja na gunia 10 za mahindi, dumu saba za maji, mafuta ya kupikia dumu tatu na vyombo vya kupikia.
Naye mmoja wa waathirika wa nyumba kuchomwa, Lucy Jacob amewashukuru Laigwanani kwa msaada huo kwani wako katika maisha magumu kwa sasa na wamemwomba Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Stephen Kiruswa kuwakumbuka na ikibidi kuwasaidia kwa namna moja ama nyingine.