Wazee waja na mkakati kulinda maadili
BARAZA la Wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Iringa limevitaka vyama vya siasa kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na mapenzi ya jinsia moja kwa kuwaibua na kuwaripoti viongozi wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo.
Wakizungumza na wanahabari leo, wazee hao wamewataka wanachama wa vyama hivyo kutoa taarifa za watu hao kwa kamati zao za nidhamu na maadili kama moja ya mikakati ya kupinga vitendo hivyo na kuwachukulia hatua zitakazoharakisha mapambano hayo.
“Hatua za mapambano haya kwa viongozi zinapaswa kwenda mbali kwa kuwalazimisha kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya vyama vyao,” alisema Mwenyekiti wa baraza hilo, Amani Mwamwindi.
Mwamwindi aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa ya Iringa kwa zaidi ya miaka 15, aliitaka jamii kuhusishwa moja kwa moja katika mapambano hayo aliyosema yakichukuliwa kwa wepesi vita yake itakuwa ngumu sana siku za usoni.
“Ulawiti, ubakaji na mapenzi ya jinsia moja ni vitendo hatarishi kwa afya ya binadamu na vinazidi kupamba moto,” alisema huku akizungumzia taarifa za ubakaji na ulawiti ambazo kwa siku za karibuni zimekuwa hazikauki katika vyombo mbalimbali vya habari.
Alisema wao kama wazee wanakemea na wanalaani vitendo hivyo wakisema vinachochewa na imani za kishirikina, mitandao ya kijamii na misimamo ya baadhi ya nchi za Magharibi.
Kwa upande wa wazazi, walezi na jamii alisema kwa pamoja wameteleza na kuacha vitendo hivyo vikizidi kushamiri na kuonekana vya kawaida katika jamii.
“Mambo haya yakichukuliwa poa kuna hatari Taifa likajikuta linakosa kizazi kipya cha kuja kuliendeleza maana hatutakuwa na ndoa na vizazi vipya, tuamke na tuingie kwenye mapambano,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya Mstaafu, Pascal Muhongole, ambaye ni mjumbe wa baraza hilo alisema kazi ya kupambana na ushoga isiachwe kwa viongozi wakuu wa serikali na dini, iende hadi ngazi ya mtaa na vijiji na ihusishe wadau wengine.
Muhongole aliitahadharisha jamii kuacha kuiga tamaduni zote za kigeni akisema zile zenye athari kwa mila, desturi na tamaduni zao ni lazima zikemewe.
“Huu ni utamaduni wa wapi wa wanaume kuoana na wanaume wenzao au wanawake kuoana na wanawake wenzao.
Kwa kufuata utamaduni huo mnataka Watanzania wenzetu wapate nini kama sio kuua uzao na kupandikiza laana katika Taifa,” alisema.
Aliipongeza serikali kwa kuendelea kuchukua hatua zinazolenga kushughulika na changamoto hiyo hata hivyo akasema juhudi hizo zinatakiwa kuongezewa nguvu ya kisheria, ili kuleta mafanikio ya haraka.
Naye Yahaya Kapela alizungumzia aina mpya ya maisha akisema yamechochewa na tamaduni za kigeni na kusababisha kuharibika kwa mila, tamaduni na desturi yetu.
“Angalia hii leo vijana wetu wa kike na kiume wanavyovaa; baadhi yao wanavaa nusu uchi kabisa na matokeo yake yameongeza vitendo hivyo hatari,” alisema na kutaka wazazi, walezi na jamii kutimiza wajibu wao katika kuwanusuru.