Wazee walalamikia kupuuzwa mabaraza ya madiwani
BARAZA la Taifa la Wazee limeeleza kusikitishwa na baadhi ya mabaraza ya madiwani nchini kupuuza sera na muongozo wa kutoa nafasi ya wajumbe wawili kutoka baraza la wazee kwenye vikao vyao.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Wazee, Lameck Sendo amebainisha hayo leo wakati akizungumuza katika kongamano la wazee kitaifa lililofanyika mjini Geita huku akiiomba serikali kukemea tabia hiyo.
Alisema sera ya wazee iko wazi inaelekeza halmashauri zote nchini kuwa na wawakilishi wawili ambao wanaingia kwenye baraza la madiwani lakini cha kushangaza halmashauri zingine zinapuuza muongozo.
“Ndiyo hao wakipewa muongozo wanadai maelekezo, wakipewa malekezo wanadai sheria, wakiwekewa sheria wanadai katiba mpya, tuwasaidie hao wakurugenzi hata hapa Geita kama wapo.
“Halmashauri zote nchini wahakikishe kwamba wawakilishi wa wazee katika mabaraza hayo wanaingia kwenye mabaraza yao, isiwe kwamba baraza linakuwepo halmashauri hii wengine hawafanyi hivo.
“Naweza kutaja hata mabaraza katika baadhi ya halamashauri nchini hapa wanaofanya vizuri na wanaofanya vibaya lakini siyo wakati wake.” Amesema Mzee Sendo.
Ametaja changamoto nyingine inayowakabili wazee ni wazee kudharauliwa, watoto kutojali wazee wao na kuwatosa, matunzo duni kwa wazee, wazee kuachwa upweke bila ulinzi na wazee kubakia wapweke.
Amesema sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaonyesha taifa lina wazee milioni 5.5 kutoka wazee milioni 2.5 kwa sensa ya mwaka 2012 hivo hatua zichukuliwe kuimarisha ulinzi, haki na heshima.
“Tuone nafasi zetu wazee katika vyombo vyenye maamuzi, kukuza uchumi wetu, maadili na malezi katika jamii na jinsi gani mabaraza yote nchini yanafanya kazi kwa kushirikisha jamii na wazee.”
Kamishina wa Ustawi wa Jamii, Dk Nandera Mhando amesisitiza serikali inaendelea kuboresha na kusimamia huduma kwa wazee sambamba na kupambana na uonevu na ukatili dhidi ya wazee.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini mchango wa wazee hivo ni lazima haki na nafasi ya wazee ilindwe.
“Tutaendelea kuwakumbusha waheshimiwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi waendelee kuwakumbusha wananchi pamoja na madiwani kuwapa nafasi na fursa na kulinda haki za wazee wetu.”