Waziri aishauri serikali kuwekeza sekta zisizo rasmi

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shabaan ameishauri serikali kuwekeza kwenye sekta isiyo rasmi ili kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wan chi, tofauti na ilivyo sasa wenye uwezo ambao ni wachache ndio wachangiaji wakubwa kwenye uchumi.

Kiongozi huyo ametoa ushauri huo Novemba 8, 2023 katika kongamano la 27 la mwaka linalojadili masuala ya utafiti. Amesema sekta isiyo rasmi ni kubwa lakini imekuwa haina tija kwenye ukuaji wa uchumi kwa sababu uchangia wake kwenye pato la taifa sio mkubwa.

“Unaweza ukawa na sekta isiyo rasmi kubwa lakini haitoi mchango wenye maana na ndio maana ukiangalia nafasi ya uchumi wetu unakuta ni wachache sana wakubwa ndio wanachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi lakini una sekta isiyo rasmi kubwa, lakini haichangii ipasavyo kwenye uchumi, hivyo muhimu kuiwekeza,” amesema.

Advertisement

Amesema sekta ya uzalishaji inakimbilia kwenye mfumo usio rasmi kwa kuwa sekta rasmi ina mifumo mingi ya udhibiti kwa hiyo watu wanaona wakimbilie sekta isiyo rasmi.

Amesema uwekezaji kwa mtaji wa watu ni muhimu katika sekta isiyo rasmi ambayo inatoa huduma, inafanya biashara ambayo inatakiwa iwekezewe kwenye ujuzi, ktaaluma mbalimbali ili nchi iendelee badala ya kufanya biashara kwa mazoea.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako akimwakilisha Makamu wa Rais, Philip Mpango amesema mambo muhimu ya kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi ni uwekezaji katika rasilimali watu.

Amesema utafiti unazungumzia kuwa ukitaka kuwa na mageuzi makubwa lazima uangalie zile sekta zinazogusa watu wengi kwa Tanzania kilimo ndio kimechukua nafasi kwa kuwa takribani asilimia 70 ya watu wako kwenye sekta hiyo.

“Katika nchi yetu tunachukulia kilimo kama sehemu ya mkakati wa kuweza kukuza nchi yetu ndio maana serikali sasa hivi imewekeza bajeti ya kilimo imekuwa takriban mara nne ya ile iliyokuwepo kabla.

“Tunawekeza katika kilimo kwa kwenda katika kilimo cha kisasa lakini pia kilimo cha umwagiliaji,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari amesema uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa kiwango cha takribani asilimia sita japo kumekuwepo mitikisiko ambayo imesababisha ukuaji ule ukapungua kwa miaka michache ilopita lakini sasa unaelekea kurudi kule ambako ulikuwepo.

“Moja ya tatizo ambalo linafanya ukuaji wa uchumi usiwe na matokeo mazuri sana katika kujenga ajira na kupunguza umaskini ni muundo wa uchumi,

“Katika Kongamano linaloendelea wameitwa wataalam mbalimbali, watunga sera na watafiti kwa pamoja kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kubadilisha muundo wa uchumi wetu ili ukue kwa kasi lakini uweze kuwa jumuishi lakini ili pia uweze kuwa endelevu kiasi kwamba misuko suko ikitokea isiweze kupunguza ile kasi ya ukuaji wa uchumi,” amesema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *