Waziri avunja Kamati ya Mipango Miji
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula, amevunja Kamati ya Mipango Miji ya Jiji la Mwanza.
Kamati hiyo ilikuwa chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Mipango miji wa Jiji la Mwanza Hamidu Said na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Yahya Sekieti, ambaye alikuwa Katibu wa Kamati.
Dk Mabula ametoa uamuzi huo leo, wakati wa kikao kazi cha viongozi wanaosimamia sekta ya ardhi kwa ngazi zote kuanzia wilaya , mitaa, kata na mkoa wa Mwanza.
“‘ Kamati zote za mipango miji na zile za uchumi, serikali ni moja tumefanya mawasiliano na leo tunaenda kuchukua maamuzi magumu.
“Kwa ushauri pamoja na Waziri wa Tamisemi, Kamati ya Mipango Miji ya Jiji la Mwanza inaenda kuvunjwa na hakuna mjumbe hata mmoja atakaetakiwa kurudi tena kwenye kamati ile, ” Dk Mabula amesema.
Amesema Mkoa wa Mwanza kumekuwa na tatizo kubwa la kudhulumu ardhi kwa wazee na wajane na kwamba kumekuwa na tatizo la utoaji vibali vya ukarabati wa majengo umekuwa unakiukwa.
Amezitaka halamshauri zote nchini kutenga maeneo ya uwekezaji na kuyalinda kwa ajili ya kupokea wawekezaji.
Ameagiza viongozi wa kuanzia ngazi ya mtaa, kata tarafa, wilaya mpaka mkoa kwa kila mwenye dhamana kutatua migogoro ya ardhi.
”Suala la utatuzi wa mgogoro wa ardhi sio suala la wizara eti kusema kuna mawaziri nane, nitashangaa eneo lina mamlaka, halafu mtu anasubiria Waziri, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, shughulikieni migogoro ya ardhi ktk maeneo yenu,” amesema DK Mabula.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema Kamati za Ardhi zina shida sana na amemuomba Waziri Dk Mabula kushugulika na Wilaya ya Nyamagana kisha wilaya ya Ilemela.