Waziri Aweso atoa maagizo maji safi
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Maji safi na Usafi wa Mazingira nchini, kushughulika na changamoto za wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma bora za maji safi.
Aweso amesema hayo leo Septemba 21, 2022, wakati akifunga kikao kazi cha Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Maji nchini mjini Morogoro.
Waziri Aweso amesema serikali imelenga kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa Watanzania wote, inafikia asilimia 95, ifikapo mwaka 2025.
Aweso amesema kufikia lengo hilo la serikali, miradi mbalimbali ya maji inatekelezwa katika kila jimbo nchini na ile ya programu ya Covid-19, ambapo tayari mamlaka za maji nyingi zimeweza kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji safi.
Hivyo amezielekeza mamlaka zile ambao hazijakamilisha miradi yao wakamilishe kwa haraka.
Waziri Aweso amewataka kwenda kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma za maji safi, kuboresha hali ya usafi wa mazingira pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji.
“Ninawaelekeza kutumia fursa hii vizuri kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa huduma za maji safi na kuboresha huduma ya maji taka katika maeneo tunayoyahudumia,” amesema Aweso.