Waziri Mchengerwa azindua tamasha la utamaduni

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amezindua Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania linalotarajiwa kufanyika nchini kwa wiki moja.

Tamasha hilo litakalofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Zanzibar linalenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tamasha usiku wa kuamkia leo, jijini Dar es Salaam Waziri Mchengerwa amesema Tamasha la Msimu wa Utamaduni ni jukwaa muhimu la kuonesha na kutangaza bidhaa za kiutamaduni za kiafrika kupitia maonesho ya kazi za mikono za utamaduni na ubunifu, matembezi ya kiutamaduni, muziki wa kiafrika pamoja na ngoma za asili.
Aidha aliongeza kuwa Tamsha hilo linadhihirisha ushirikiano wa muda mrefu wa nchi hizi mbili ambapo Tanzania na Afrika Kusini umedumu kwa muda mrefu huku akisema kuwa uhusiano huo uliasisiwa na wazee ambao ni Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Nelson Mandela wa Afrika Kusini toka enzi za kupigania uhuru.

“Wakati wa harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika, Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ilikuwa ngome na kitovu cha harakati za kupigania uhuru. Vyama vya ukombozi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo ANC na PAC vya Afrika Kusini vilipata mafunzo ya kupigania uhuru nchini Tanzania kutoka mwaka 1964-1994.” Alieleza

Waziri huyo aliongeza na kusema kuwa nchi hizo mbili zimeendelea kuwa na urafiki na ushirikiano katika Sekta mbalimbali ikiwemo Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Akifafanua juu ya tamasha hilo alisema litajumuisha shughuli mbalimbali za Sanaa na Utamaduni ikiwemo, Maonesho ya harakati za Ukombozi, Sanaa za ufundi za Afrika Kusini na Tanzania, ngoma za asili, maonesho ya filamu za Tanzania na Afrika Kusini, uchoraji wa kiubunifu na kutembelea maeneo yenye historia ya Ukombozi wa bara la Afrika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma.

“Hii itawapa wageni na watanzania fursa ya kujifunza historia ya mapambano ya kudai uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika na kujionea urithi mkubwa wa historia uliosalia katika nchi yetu,” aliongeza

Habari Zifananazo

Back to top button