Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kikao cha pamoja na Mawaziri wa Kisekta, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na wilaya za Morogoro cha kujadili changamoto za usimamizi wa ardhi kitatoa mwelekeo wa kutekelezwa nchi nzima kwa kuthibiti uharibifu wa vyanzo vya mazingira na vyanzo vya maji na kutaka kila kiongozi kuwajibika kwa nafasi yake.
Amesema haikubaliki kwa sekta moja inaleta athari kubwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali wapo na ikizingatiwa matumizi ya ardhi yametolewa maelekezo ya kisheria na kinachotakiwa ni namna ya utekelezaji na nini kifanyike.
“ Nini cha kufanya ili kudhibiti changamoto kwenye sekta ya mifugo , mifugo ni maisha , mifugo ni uchumi , mifugo ni fursa , mifugo ni pato la mtu mmoja mmoja na Taifa pia “ amesema Waziri mkuu na kuongeza.
“ Ni lazima twende pamoja tuweze kuratibu ili yale yote tuliyotamka yaweze kuleta manufaa makubwa kiuchumi yanayotokana na mifugo na kama maisha pia yanatokana na mifugo, fursa za uwekezaji kwenye viwanda turatibu vizuri mifugo ilete viwanda kupitia malighafi ya mifugo” amesema Waziri Mkuu.