WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuharakisha mchakato wa kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia nchini.
Majaliwa ameyasema hayo Septemba 20, 2023 mara baada ya kutembelea banda la PURA kwenye kongamano la nishati linaloendelea kwa siku mbili katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Hakikisheni mnaongeza kasi katika mchakato wa kunadi vitalu vyetu ili wawekezaji waje kuwekeza katika utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini ili nchi inufaike,” aliongeza.
Akitoa taarifa fupi mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni alieleza kuwa Mamlaka inaendelea na shughuli za awali za utekelezaji wa duru ya tano ya kunadi vitalu vya mafuta na gesi kwa maeneo ya nchi kavu na baharini kwa lengo la kuongeza wawekezaji.
Aliongeza kuwa sambamba na maandalizi hayo PURA inaendelea kuweka mipaka ya vitalu vitakavyonadiwa na kuandaa vifurushi vya data (Data Packages) kwa kila kitalu.
“Hadi sasa vitalu 26 vinafanyiwa uchambuzi ili kupendekezwa kwa ajili ya kuingizwa katika mnada. Kati ya hivyo, vitalu 15 vipo nchi kavu na 11 vinapatikana baharini,” alifafanua Mhandisi Sangweni.
Alibainisha pia kuwa Serikali inatarajia kuzindua zoezi la kunadi Vitalu kati ya mwezi Desemba, 2023 hadi Machi, 2024 baada ya kukamilika kwa shughuli za maandalizi zinazoendelea.
Inaelezwa kuwa zoezi la kunadi vitalu linakadiriwa kugharimu jumla ya Shilingi bilioni 3.5.
Aidha, kwa mwaka 2023/24 Serikali kupitia PURA imetenga Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kazi za awali za maandalizi ya zoezi hilo.