Waziri Mkuu ampa Sh milioni 1 mvuvi ‘shujaa’ uokozi Precision Air
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa mkono wa pongezi wa Sh milioni 1 kwa mvuvi aliyefahamika kwa jina la Majaliwa ambaye anatajwa “shujaa” wakati wa uokozi wa watu waliokuwa katika ndege ya Precision Air iliyoanguka Ziwa Victoria na kuua watu 19 akiwemo rubani wa ndege.
Majaliwa anadaiwa kutumia kasia yake kuvunja mlango wa dharura wa ndege hiyo na kuwezesha kuokoa watu 24 waliokuwa katika ndege hiyo. Hakuwa na elimu ya uokozi na wala hajawahi kupanda ndege.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amesema kijana huyo alikuwa mtu wa kwanza kufika katika ndege hiyo dakika chache tu baada ya kuanguka katika Ziwa Victoria kwa kushindwa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba.
Chalamila amemuomba Waziri Mkuu Majaliwa kusaidi kiasi cha fedha kutoka mfuko wa maafa kwa ajili ya kufundisha wavuvi hatua za awali za uokozi.
Waziri Mkuu anaongoza mamia ya wakazi wa Kagera, Ndugu jamaa na marafiki waliohudhuria katika hafla ya kuaga miili ya marehemu 19 wa ajali ya ndege ya Precision air.
Tembo Nikel wamechangia Sh milioni 10, Kiwanda cha Kagera Sugar kimechangia Sh milioni 1 kwa kila familia ya mfiwa. Precision Air wamechangia Sh milioni 2 kwa umoja wa wavuvi. STAMIGOLD imechangia pia Sh 500,000 kwa kila mfiwa.