Waziri Mkuu kuanza ziara Geita kesho

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

GEITA: WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa anatarajiwa kuwasili mkoani Geita Ijumaa Mei 31, 2024 kwa ajili ya ziara ya siku tatu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela ametoa taarifa hiyo leo na kuelezea kuwa Waziri Mkuu atawasili Uwanja wa Ndege wa Chato na atapata nafasi ya kukutana na kufanya mazungumuzo na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato.

Amesema pia mkutano huo utajumuisha watendaji na wakuu wa taasisi ndani ya Mkoa wa Geita, ambapo kikao hicho kitafanyika katika ukumbi wa halmashauri wilayani Chato.

Advertisement

Ameeleza, Juni mosi, 2024 Waziri Mkuu atashiriki maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Kanda ya Ziwa na kisha kuweka jiwe la msingi katika soko la samaki na baadaye kuzungumza na wananchi.

“Kwenye kanda yetu ya Ziwa Viktoria Mheshimiwa Kassimu Majaliwa atakuwa mgeni rasmi ambapo maadhimisho yetu yatafanyika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato,” amesema Mkuu huyo wa mkpa.

Amesema Juni 2, 2024 Waziri Mkuu ataelekea wilayani Nyang’hwale na kuweka jiwe la msingi katika jengo la halmashauri ambalo limekamilika ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Waziri Mkuu ataelekea kwenye jengo la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililojengwa mji wa Kalumwa na kisha kufanya mkutano wa hadhara Uwanja wa Sabasaba utakaoanza saa nne asubuhi,” amesema.