Waziri Mkuu wa Ethiopia kufanya ziara ya siku tatu

DODOMA: WAZIRI Mkuu wa Ethiopia, Dk Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia Februari 29, hadi Machi 02, 2024 kwa mwaliko wa Rais, Dk Samia Suluhu Hassan.

Taarifa iliyotolewa leo mjini Dodoma na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeeleza kuwa  Dk Abiy atapokelewa rasmi Ikulu, Dar es Salaam Machi Mosi na mwenyeji wake Rais Samia.

“Lengo la ziara hii mbali na kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, inalenga pia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ethiopia ambazo zimekuwa zikishirikiana katika maeneo ya biashara na uwekezaji, elimu, utamaduni,

usafirishaji wa anga, kilimo, mifugo, udhibiti wa uhamiaji holela, ulinzi na usalama.” Imeeleza taarifa hiyo.

Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta ya anga ambapo mwaka 2016 hadi 2023 jumla ya marubani 75 na wahandisi 25 kutoka Tanzania wamepokea mafunzo katika ngazi tofauti nchini Ethiopia. Hivyo ni wazi kuwa, ziara hii itafungua milango zaidi ya ushirikiano kati ya Shirika la Ndege la Ethiopia na Shirika la Ndege la Tanzania – ATCL katika kujiendesha kibiashara.

Tanzania na Ethiopia zina uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wa kihistoria ambao ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia, Hayati Haile Selassie. Viongozi hawa walishirikiana bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na ni miongoni mwa Viongozi Waanzilishi 32 wa Umoja wa Afrika wakati huo (OAU) mwaka 1963.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button