Waziri Silaa ang’ata mapapa wa ardhi

DODOMA; WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amehitimisha mjadala wa hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake na kusema hatarudi nyuma hadi ahakikishe mapapa wa ardhi wote wamefikishwa katika vyombo vya sheria na sekta ya ardhi ikiwa salama.

Waziri Silaa ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Mei 27, 2024, alipokuwa akifanya majumuisho ya hotuba yake aliyoiwasilishwa bungeni Mei 24, 2024 akisema kuwa sekta ya ardhi kuna changamoto nyingi na kwamba hali ikiachwa ilivyo Watanzania wengi wanyonge watakosa haki zao.

Amesema kwa muda wote ambao atakuwa kwenye wizara hiyo atasimamia haki bila kumuonea mtu na kusisitiza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha matapeli wote wanapatikana na wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Amesema wataendelea na kliniki ya ardhi ambayo sasa itajulikana kama Samia Ardhi Kliniki, ambayo itakuwa maalum kuwafuta machozi Watanzania wote.

Waziri Silaa pia ameonya wasimamizi wa mirathi kwamba hawatakiwi kuuza mali za mirathi kwani kufanya hivyo ni kuwadhulumu watoto wa marehemu.

Wakati akiwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Mei 24, 2024 jijini Dodoma, Waziri Silaa alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi mijini na vijijini, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma na upatikanaji wa taarifa za ardhi.

Vipaumble vingine ni kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuimarisha mipaka ya kimataifa. Bunge limepitisha bajeti hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button