Waziri Tabia atoa baraka michezo ya bandari

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Tabia Maulid Mwita amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni , Sanaa  na Michezo Tanzania Bara, wamejipanga kuhakikisha wanaendeleza sekta ya michezo, ili kuleta ushindani wenye tija kimataifa.

Waziri Mwita  alisema hayo, jana Septemba 26, 2022 katika hotuba ya  ufunguzi wa michezo ya 16 ya Bandari (Interports Games ) ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA,  katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro inayoshirikisha wanamichezo zaidi ya 500.

Alisema zipo jitihada za wazi kwa wizara zote mbili katika suala la kuwajengea uwezo wanamichezo,  ili waweze kufanya vizuri kwenye  mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa maslahi ya Watanzania.

Waziri Mwita alisema kwa  Zanzibar,  wizara yake imeamua kufufua mashindano ya wizara ambayo yalianza mwaka jana, katika  ngazi za wizara pekee na kwa mwaka huu  imejipanga kuzishirikisha taasisi mbalimbali za serikali.

Alisema ili  kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi, umoja wa kitaifa na kudumisha muungano, wizara yake itashirikiana na wakurugenzi wa bandari wa pande zote mbili  Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara kuona uwezekano  mashindano ya mwakani yafanyike Zanzibar.

“ Kufanyika kwa michezo ya bandari  inayoshikisha na upande wa Zanzibar inatoa fursa ya kuimalisha undugu wetu uliopo na Muungano ambao umeasisiwa muda mrefu, “ alisema Waziri Mwita

Naye   Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mkeli Mbossa,  kwenye  hotuba yake iliyosomwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Juma Kijavara, alisema  mamlaka hiyo  inatambua umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya za wafanyakazi.

“Nisisitize tu kwa wafanyakazi wetu wote ni vyema kufanya mazoezi hata kama hakuna michezo hii ya Interports, “  alisema Kijavala

Habari Zifananazo

Back to top button