Waziri Tamisemi asifu utendaji wa Rais Samia
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI ) Angela Kairuki amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kubadilisha wizara na taasisi zake zinazosimamia utumishi wa walimu kwa kuzipa fedha pamoja na vitendea kazi.
Kairuki ametoa pongezi hizo leo Agosti 14, 2023 katika hafla ya awamu ya tano ya kukabidhi magari kwa maafisa elimu sekondari wa halmashauri nane.
Halmashauri zilizopewa magari hayo ni Hai, Mtama, Songea Manispaa, Bukoba vijiji, Monduli, Handeni, Ikungi, Sumbawanga Manispaa na magari mawili kwa ajili ya ofisi ya Tamisemi.
Amesema, kuanzia Machi mpaka Juni 2023 Rais Samia ametoa Sh bilioni 207.9 kwa ajli ya kulipa stahiki na madeni mbali mbali ya watumishi 121,858,000.
Kairuki amesema kwa Dar es Salaam, mradi wa shule za awali na msingi ‘BOOST’ wametenga Sh trilioi 1.15 upande wa mradi wa uhimarishaji mazingira ya kujifunzia Sequip kwa ajili ya sekondari ametenga sh trilioni 1.2 sambamba na ujenzi wa miundombinu kwa shule za kutwa msingi na sekondari ili wanafunzi wanaoripoti wasikutane na changamoto ya aina yoyote.
Aidha, Kairuki amewataka wakurugenzi kusimamia kwa karibu ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari unaoendelea kwenye maeneo yao nchi nzima hasa ya kidato cha tano ili wanafunzi walioanza kuripoti leo Agosti 14, 2023 wakute mazingira rafiki ya kujifunzia.
Amesema,serikali kupitia programu ya lipa kulingana na matokeo katika sekta ya elimu (EP4R) imenunua magari 200 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya maafisa elimu wa sekondari wa halmashauri na ngazi ya wizara.
Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayesimamia elimu, Charles Msonde amesema malalamiko ya walimu kupandishwa madaraja tayari wameshashughulikia wengine wameshapandishwa na wengine wanaendelea kupandishwa lengo ni wote wapande
“Tunafanya kazi kupitia horodha ya walimu wote, jina kwa jina kichwa kwa kichwa, hakuna atakayeachwa kama walitakiwa kupanda kwa mujibu wa mwongozo baada ya miaka minne waonyeshe walikuwa wapi…;
“Kabla ya Disemba mwaka huu walimu wote watakuwa wamewekwa kwenye madaraja sahihi ili waingizwe kwenye mfumo wa bajeti mwaka mpya wa fedha 2023/2024 mwakani ili tunapoanza mwaka mpya wa fedha kusiwe na malalamiko ya changamoto za walimu.
Amesema, kwa sasa Tamisemi imefanya maboresho makubwa na hakutakuwa na ucheleweshaji wa kupandishwa madaraja.