Waziri Ulega atoa maelekezo uvuvi haramu

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega amemuagiza Mkurugenzi wa Uvuvi, Profesa Mohamed Sheikh kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanakomesha vitendo vya uvuvi haramu katika ukanda wa Pwani.

Pia ameagiza wavuvi kupangwa vyema,watambuliwe kwani mahitaji ya boti ni makubwa kwa kundi hilo.

Ulega ametoa maagizo hayo leo Dar es Salaam wakati wa hafla ya ugawaji wa boti za kisasa kwa wavuvi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Boti hizo zinatolewa kwa mikopo chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Katika awamu ya kwanza jumla ya boti 160 zenye thamani ya Sh bilioni 11.5 zitatolewa kwa wanufaika nchi mzima.

” Labda kuna ulegevu wa wasimamizi wangu mahali, sasa tumefungua ukurasa mpya na kwa vile hatukuwa na Mkurugenzi wa kushughulikia eneo hilo kwa Sasa linepata tiba,” amesema akizungumzia suala la uvuvi haramu.

Kuhusu kuwatambua wavuvi amesema endapo wavuvi wataonekana ni watu waaminifu, watu wengi zaidi watajitokeza kuwakopesha.

“Tunajua mahitaji ya samaki ni makubwa lakini njia mnazotumia kuvua hamuwezi kupata mazao mengi zaidi, tayari zimeshaidhinishwa fedha nyingine Sh 11 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa boti nyingine,”amesema.

Hata hivyo Ulega amewatahadharisha wavuvi na kuwataka wakatumie boti hizo kwaajili ya ujenzi wa uchumi na familia zao, badala ya kuendeleza malumbano kwenye vikundi vyao na kwamba mchango wa uvuvi unalenga kufikia asilimia 1.8 ifikapo mwaka 2030.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Riziki Shemdoe amesema utoaji wa boti hizo ni mpango wa kuwawezesha wavuvi wadogo katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Profesa Shemdoe amesema jumla ya boti 92 zitatolewa katika ukanda wa Pwani na 27 katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button