Waziri Ummy afafanua bima ya afya kwa wote

Waziri Ummy afafanua bima ya afya kwa wote

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuelekea mpango wa bima ya afya kwa wote, hakuna mwananchi atakayelazimishwa kupata bima kwa kupewa adhabu kama vile kutozwa faini au kukamatwa.

Akizungumza leo katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema wataweka utaratibu maalum, ili kuhakikisha wananchi wanajiunga katika mfuko huo

Amesema kupitia mfumo wa bima ya afya kwa wote, mfumo wa rufaa wa matibabu utatumika, ambapo wananchi watapata matibabu kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Taifa itakapohitajika.

Advertisement

“Niseme tena hakuna Mtanzania atafungwa au kukamatwa kwa kutokuwa na bima ya afya, hakuna hicho kifungu, lakini tunawapataje Watanzania ambao hawaumwi kujiunga na bima ya afya, ndio maana tumefungamanisha bima na baadhi ya huduma,”amesisitiza.

Ummy amesema miongoni mwa huduma hizo ni kama  leseni ya biashara, leseni ya udereva  na mengine.

Amesema lengo la serikali kuja na bima ya afya kwa wote ni kuwapunguzia mzigo wananchi kwenye matibabu.

Ummy amesema kuwa si lazima watanzania wote wajiunge na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), kwani kutakuwa na wigo mpana wa wananchi kuchagua taasisi waitakayo.

” Kama vile bima ya gari, unataka kuwa na gari lako lazima uwe na bima, kwa hiyo unaweza kuwa na binafsi au ya serikali.

“Lakini sisi sasa lazima uwe na bima ya afya, muswada tunapendekeza kuwe na  kitita cha mafao chenye usawa, ambacho kila atakayejiunga na  bima ya afya atakuwa na haki ya kupata,” amesema.

1 comments

Comments are closed.