WIZARA ya Afya imekiri kuwepo uzembe katika utoaji wa chanjo za magonjwa mengine ikiwemo surua kutokana na ukweli kuwa nguvu nyingi zilielekezwa katika chanjo ya UVIKO-19 na kusahau chanjo za magonjwa mengine.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo leo Februari 24,2023 kwa nyakati tofauti, wakati akizungumza na wananchi katika mji mdogo wa Usevya na Kata ya Majimoto Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi katika mkutano wa hadhara alipofika kuzindua chanjo na kutoa salamu za pole.
Amesema hali hiyo imeleta madhara kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa surua nchini, na kusababisha vifo vya watoto 13 wilayani Mlele hadi kufikia jana Februari 23, 2023.
“Katika kipindi cha miaka mitatu tumesuasua katika kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua katika nchi hii, tumebaini kwamba kuna watoto zaidi ya 400,000 nchini Tanzania hawajapata kabisa chanjo ya dozi ya surua,” amesema.
Amesema hadi sasa ugonjwa wa surua umebainika katika Wilaya 19 za Tanzania bara ambazo ni Nsimbo, Tanganyika, Mpanda, Chunya, Bagamoyo, Kisarawe, Sikonge, Nzega, Tabora Manispaa, Kalambo, Sumbawanga, Sumbawanga Manispaa, Malinyi, Ulanga, Muleba, Korogwe, Mtwara Manispaa na Uvinza ambapo kati ya Wilaya hizo wilaya iliyoathirika zaidi ni Mlele Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Amesema katika halmashauri hiyo kati ya wagonjwa 100 waliopata surua, wagonjwa 45 wametoka katika Kata ya Majimoto.
Katika kuhakikisha watoto wote nchini wanapata chanjo ya ugonjwa huo, Waziri Ummy amesema serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuhakikisha chanjo zinapatikana za kutosha, kutoa kampeni nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano anafikiwa na amewaagiza wakuu wa mikoa nchini kuwatafuta watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano, ambao hawajapata chanjo ya surua kuhakikisha wanapata chanjo.
Amesema kwa mujibu wa sheria ya afya ya jamii endapo mzazi au mlezi atabainika kutompeleka mtoto kupata chanjo anaweza kutozwa faini ya shilingi 100,000 au kifungo cha miezi mitatu gerezani au vyote kwa pamoja.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy ameitaja mikoa 20 ya Tanzania Bara ambayo watoto wengi bado hawajakamilisha dozi ya pili ya chanjo ya ugonjwa wa surua ni Katavi, Tabora, Dar Es Salaam, Arusha, Geita, Rukwa, Shinyanga, Manyara, Tanga, Lindi, Songwe, Mtwara, Iringa, Singida, Ruvuma, Dodoma, Kigoma, Morogoro na Mbeya na kuwataka viongozi kusimamia ipasavyo jambo hilo.