Waziri Ummy: Madaktari bingwa kutawanywa upya

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali inakusudia kuwatawanya upya (re-distribute), madaktari bingwa ili kukabili uhaba wa wataalamu hao kote nchini.

Akitoa ufafanuzi wakati wa kipindi cha maswali bungeni leo Aprili 18, 2023, Waziri Ummy amesema Wizara ilipata kibali cha ajira mwaka jana, hata hivyo hawakuweza kupata madaktari bingwa kutokana na uhaba wa wataalamu hao sokoni.

“Tulipata kibali cha kuajiri madaktari bingwa, lakini hatukuwapata sokoni. Kwa sasa mkakati ni kuwatumia madaktari waliopo katika hospitali husika kwa kuwasomesha, kwa bahati mbaya hawajamaliza,” amesema Waziri Ummy.

Advertisement

“Tumefanya tathmini ya madaktari bingwa na tumegundua baadhi ya hospitali za rufaa za mikoa zina madaktari bingwa wengi kuliko hospitali nyingine na hivyo tunafanya kuwatawanya upya,” amesema.

Waziri Ummy amesema wizara imepata pia kibali cha ajira ya madaktari bingwa kwa mwaka huu. Hakusema ni lini zoezi la kuajiri litafanyika ingawa ameeleza zoezi la kuwagawanya madaktari bingwa waliopo limeathiriwa na uhaba wa fedha.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya amesema serikali imeanza kutekeleza mpango wa ‘Samia Suluhu Super Specialist’ kusomesha madaktari bingwa zaidi ya 400. Mpango huo serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 8 kwa ajili ya kusomesha madaktari hao ndani na nje ya nchi.