Waziri Ummy: Uzee na kuzeeka havikwepeki

.....amewataka wabunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Ijumaa, wazee bila kikwazo chochote

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka wabunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Ijumaa, wazee bila kikwazo chochote huku akisisitiza “uzee, kuzeeka hakukwepeki.”

Waziri Ummy ametoa wito huo leo Jumanne bungeni Dodoma leo wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy, Wizara anayoiongoza inaamini kuwa kupitishwa kwa Sheria ni hatua muhimu itakayolisaidia kundi hilo kupata dawa bila vikwazo vyovyote.

Amelazimika kuwashawishi wabunge kuupitisha muswada huo baada ya Mbunge wa Lushoto, Shaban Shekilindi aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kuboresha huduma ya afya kwa wazee.

Ummy ameliambia Bunge kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya za wazee.

“Kwa miaka mingi wazee wamekuwa wakipatiwa huduma mahsusi kwa kupitia madirisha maalum ya huduma za afya kwa wazee yaliyotengwa katika vituo vya kutolea huduma,” ameeleza.

Akifafanua zaidi, Waziri amesema katika mwaka huu wa fedha, 2022/2023 muundo mpya umepitishwa ambao unaiwezesha Wizara kuanzisha seksheni ndani ya kurugenzi ya Tiba

inayoshughulika na Huduma za Afya ya Wazee (Geriatrics), Huduma za Utengamao (Rehabilitation services) na Huduma za Tiba Shufaa (Palliative Therapy).

Kupitia seksheni hiyo, Waziri ameeleza, uratibu wa huduma/afua mbalimbali za afya ya wazee utafanyika na maboresho ya huduma za afya kwa wazee yatapokelewa na kuchakatwa na kupatiwa majawabu kwa wakati.

Rasimu ya mwongozo wa utekelezaji wa mkakati wa huduma za afya kwa wazee ipo katika ngazi ya maboresho hivi sasa.

Waziri amemalizia jibu lake kwa kusema: “Uzee na kuzeeka havikwepeki, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea Kuwaenzi Wazee Wetu.”

Habari Zifananazo

Back to top button