‘Wekeni mazingira mazuri ya biashara EAC’

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, amesema  umefika wakati kwa mamlaka mbalimbali za serikali kuweka mazingira mazuri ya Watanzania kufanya shughuli za kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambako Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imejumuishwa.

Amesema hakuna sababu ya kuwepo vikwazo vingi, ambavyo vitasababisha wananchi kushindwa kutumia fursa zilizopo kwenye jumuiya hiyo, huku akieleza kuwa Tanzania imebahatika kupakana na nchi nane, jambo ambalo ni fursa kubwa kiuchumi.

Akizungumza  na  wana CCM na wananchi wa Kagera, Kinana amesema  hivi karibuni DRC imejiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hatua ambayo imetanua fursa ya soko eneo la jumuiya hiyo.

“Hivi karibuni kulikuwa na mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakajiunga pale. Congo DRC ukubwa wake ni mara mbili ya Tanzania, idadi ya watu wake ni mara mbili yetu sisi, mahitaji yao ni mara nne yetu, utajiri wao mara 20 ya sisi, sasa kitu gani unataka zaidi ya hilo, ni fursa kubwa.

“Kuna sheria inaitwa sheria ya Afrika Mashariki ya ushuru wa forodha, ambayo inarahisisha biashara kati ya nchi wanachama na ukisoma mkataba wa ushirikiano wa nchi wanachama kuna sheria nyingine inaitwa sheria ya kuruhusu watu kutoka nchi moja kwenda nyingine, mzigo kutoka nchi moja kwenda nyingine na watu wanaotaka kufanya kazi kutoka nchi moja kwenda nyingine.

“Kwa hiyo kazi ya wabunge pamoja na viongozi ni kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zilizomo na namna sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayotoa nafasi kwa watu kufanya shughuli zao na biashara ya mipakani, Tanzania ina bahati kubwa kwani inapakana na nchi nane.”

“Tuna mipaka na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, DR Congo, kila mahali tuna mipaka na watu wanafaidi biashara ya mipakani, hivyo serikali kazi yake ni kurahisisha watu kutembea sio kupiga breki kila mahali, watakuja Wacongomani kuja kununua vitu Kigoma, halafu unamuuliza Mcongoman umekuja kufanya nini Kigoma?

“Mtu anapeleka bidhaa zake Uganda,  unamuliza unaenda wapi?  Wakiwauliza wajibuni naenda Dar es Salaam, wafanyabiashara wa kigeni wakija cha kwanza anaulizwa unaondoka lini?

“Kwa wale mnaokwenda Hongkong naamini mpo hapa, ukifika Hongkong huulizwi utaondoka lini bali wanaangalia Pasipoti yako, wanapiga muhuri wa siku 90 yaani miezi mitatu, kisha unaendelea na shughuli zako, tumia fedha zako, nunua unachokitaka ondoka.

“Niwaambie mimi ni msaidizi wa Rais najua msimamo wa Rais,  anataka kuondokana na sheria zote zinazoleta vikwazo katika shughuli za wananchi, kazi yangu na viongozi wengine ni kumpa moyo Rais kumwambia hiyo njia unayokwenda ni sawasawa,” alisema.

Alisisitiza kwamba baada ya kumaliza ziara yake atakaporudi atakwenda kumwambia Rais Samia Suluhu Hassan kwamba wananchi wa Mkoa wa Kagera wamemwambia kanyaga, apeleke bungeni sheria za hovyo ili zifutwe.

Habari Zifananazo

Back to top button