‘Wekezeni michezo ya ufukweni’

TIMU ya Taifa ya Soka la Ufukweni

DODOMA; SERIKALI imetoa rai kwa wadau wa michezo mbalimbali kama mitumbwi na ngalawa, kuogelea, mpira wa kikapu na wavu kuwekeza katika michezo ya ufukweni ili kuendeleza fukwe zilizopo.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ametoa kauli hiyo bungeni leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima aliyehoji mipango ya serikali kuitumia bahari kwa michezo mbalimbali ya majini, ili kuongeza kipato cha wananchi katika Jimbo la Kawe.

“Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995 ibara ya 7 (i-vi), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na wadau wa sekta ya michezo zikiwemo taasisi, mashirika na watu binafsi.

Advertisement

“Hata hivyo, wizara kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), wako katika mkakati wa kuziendeleza fukwe za Kunduchi na Kigamboni katika Jiji la Dar es salaam,” amesema Naibu Waziri na kuongeza kuwa lengo ni kukuza mchezo wa soka la ufukweni ambao tayari TFF wameshaanzisha ligi yake.

“Nitoe rai kwa wadau wa michezo mingine kama mitumbwi na ngalawa, kuogelea, mpira wa kikapu na wavu kuwekeza katika michezo hii ya ufukweni na kuziendeleza fukwe tulizonazo, ili kukidhi matakwa ya michezo yao kwani pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi, michezo hii pia inasaidia kuimarisha afya na kutoa burudani kwa wananchi,” amesema.

4 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *