SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kushirikisha watumishi wenye mahitaji maalumu kwenye mashindano yake ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenister Mhagama kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano hayo jijini hapa jana.
Alisema kuwa uwepo wa timu za wenye mahitaji maalumu itasaidia kuongeza wigo wa michezo, lakini na kuwawezesha watumishi wa umma wenye mahitaji maalumu nao kushiriki na kuonesha uwezo.
“Niwaombe Shimiwi kuangalia uwezekano wa kuwa na timu za wenye mahitaji maalumu ili nao waweze kupata fursa ya kushiriki katika michezo hiyo na kuongeza wigo wa michezo,” alisema.
Aidha, Mhagama alisema kuwa serikali itaendelea kutenga bajeti ya michezo hiyo ili watumishi wengi wa umma waweze kushiriki kwa wingi katika michezo hiyo. Aliwataka waajiri kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi kwa watumishi ambao ni wanamichezo kujiandaa mapema na kuleta ushindani katika michezo hiyo, badala ya kushiriki bila ya kufanya mazoezi.
“Haipendezi wanamichezo wanakuja kwenye mashindano bila ya kujiandaa, hivyo niwatake waajiri kutoa fursa ya timu zenu kujiandaa ili kuweza kuleta ushindani wenye tija kwenye mashindano haya,” alisema.